Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Dodoma na Morogoro wamepongeza Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Latifa Alhinai Mansoor baada ya kuapishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 22 Januari, 2025.
Mhe Jaji Mansoor aliteuliwa tarehe 10 Januari, 2025 na Mhe. Rais Samia kuwa Jaji wa Mahakama hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mansoor alikuwa Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Morogoro.
Akizungumza na wanachama wa TAWJA kwa Mkoa wa Dodoma na Morogoro Mhe. Jaji Mansoor amewashukuru wanachama hao kwa upendo na ushirikiano wao waliouonesha kwake.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa neema yake ya kunifanya nimetambuliwa na kunifanya niwe hivi nilivyo leo, sijui tamaduni za kule lakini ninaahidi nitafanya kazi kwa bidii kubwa ninamuomba Mwenyezi Mungu anipe afya ya kutosha ili niweze kutimiza majukumu yangu ipasavyo hasa kusimamia ukuaji, uboreshaji na utendaji kazi wa Mahakimu,” amesema Mhe. Jaji Mansoor.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amempongeza Mhe. Mansoor na kumtakia kila lakheri katika majukumu yake, na kumuomba apokee zawadi ambayo ameandaliwa na wanachama wa TAWJA wa Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya TAWJA Morogoro pamoja na watumishi wa Morogoro Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Morogoro Mhe. Susan Kihawa amempongeza Mhe. Jaji Mansoor kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuahidi wataendeleza yale mazuri ambayo amewaachia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya watumishi kutoka Dodoma na Morogoro.
TANZANIA WOMEN JUDGES ASSOCIATION.
© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved