Jumla ya Majaji na Mahakimu Wanawake 43 ambao ni wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wamewasili katika Mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini leo tarehe 08 Aprili, 2025 kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani (IAWJ) unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 09 Aprili, 2025.
Akizungumza katika mahojiano maalum leo tarehe 08 Aprili, 2025 mjini humo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema kuwa, Mkutano huo unatarajiwa kuanza rasmi kesho tarehe 09 hadi 12 Aprili, 2025 na Mgeni Rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa.
“Mkutano huu ni wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Duniani, kwa ujumla unawakutanisha wanachama Majaji na Mahakimu wanawake duniani. Kwa upande wa Tanzania tutakaoshiriki katika Mkutano huo ni wanachama 43 idadi hii imejumuisha na wenzetu wa Zanzibar,” amesema Mhe. Sehel.