Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amesema Majaji na Mahakimu Wanawake nchini wana wajibu mkubwa wa kusimamia haki za binadamu, maadili ya jamii na usawa wa kijinsia ili kuleta ustawi katika jamii.
Akizungumza jana tarehe 23 Oktoba, 2025 wakati akifungua Mafunzo kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwenye ukumbi wa Mikutnao wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju alisema kupitia mafunzo hayo ni muhimu wakaweka mikakati thabiti itakayowezesha kufikia ustawi katika jamii.
“Ninachoona ni kwamba ninyi TAWJA mnajitambua, wajibu wenu leo ni kuja na mikakati ambayo itawezesha kutatua hizi changamoto ambazo zimekuwa zinajitokeza kwenye haya masuala yanayowahusu na hasa haki za binadamu wote ambao humo wanajumuishwa Wanawake na Wanaume wakiwa wa umri mbalimbali, wengine watu wazima, wengine wazee na wengine Watoto kwa mfano kuna changamoto hii ya makosa unyanyasaji wa kijinsia,” alisema Jaji Mkuu.
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) jana tarehe 23 Oktoba 2025 kimeanza kufanya mafunzo maalum kwa Waratibu wa Kikanda wa chama hicho, ambayo yamelenga kuimarisha uongozi, usimamizi na uwajibikaji katika kulinda haki za kijinsia na za binadamu.
Mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa TAWJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo kuongeza uwezo wa Waratibu wa Mkoa katika uratibu, mawasiliano, na utekelezaji wa programu za kikanda.
“Tunatarajia kuwa kupitia waratibu hawa, TAWJA itaimarika na kuwa kinara katika ulinzi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia nchini,” alisema Mhe. Sehel.
TANZANIA WOMEN JUDGES ASSOCIATION.
© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved