Kongamano maalumu la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake limefanyika Machi 10, 2026 katika ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, Mahakama ya Tanzania na wadau wa maendeleo kujadili nafasi ya wanawake katika sekta ya utoaji haki na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera.
Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Rehema Joseph Kerefu alisema kuwa majaji na mahakimu wanawake wana nafasi muhimu katika kuimarisha utoaji wa haki unaozingatia usawa wa kijinsia na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kujitokeza katika jamii.
Alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa misingi ya kisheria na kitaaluma inayolinda haki za wanawake, bado baadhi ya mila na desturi zinazochochea mfumo dume zimekuwa kikwazo katika kufanikisha usawa wa kijinsia, huku changamoto kama ubakaji, unyanyasaji wa kingono, ukatili wa majumbani na ndoa za utotoni zikiendelea kujitokeza.
Washiriki wa kongamano hilo pia walibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuongeza uwakilishi wa wanawake katika Mahakama, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia nafasi hizo kuimarisha utoaji wa haki na kuongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla.
TANZANIA WOMEN JUDGES ASSOCIATION.
© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved