Month: May 2025

MKUTANO WA 17 WA IAWJ WAHITIMISHWA

MKUTANO WA 17 WA IAWJ WAHITIMISHWA

Mkutano wa 17 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) umehitimishwa huku wanachama wa Chama hicho wakisisitizwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.

Akifunga mkutano huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Afrika Kusini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kikatiba ya Nchi hiyo, Mhe. Nonkosi Mhlantla aliwataka washiriki wa mkutano huo kujithamini na kujipenda sambamba na kutosahau waliyojifunza wakati wote wa mkutano huo.

“Nawasihi kutosahau kupitia mliyojifunza mtapata uzoefu mzuri, Majaji mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia uzoefu wao juu ya namna wanavyoshughulikia mashauri yanayohusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake, hivyo ni muhimu kujifunza na kuyaishi yote mazuri tuliyoyapata,” alisema Mhe. Mhlantla.

Jaji huyo aliwakumbusha Majaji na Mahakimu wanawake kujipenda na kujithamini kwanza ambapo alisema, “ni muhimu kujipenda na kujithamini, kufanya hivyo sio ubinafsi bali ni muhimu kufanya hivyo ili tuwe katika nafasi nzuri ya kutekeleza vizuri majukumu yetu ipasavyo,” alisisitiza.

Aidha, Jaji Mhlantla  alisema kuwa, bado Mahakama nyingi hazina mbinu za kiusalama katika kuwalinda wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia huku na kusema kwamba kuna haja ya kuchukua hatua thabiti ili kuwalinda watu hao.

Mgeni Rasmi huyo alizikumbusha pia nchi wanachama wa IAWJ kufanya uanaharakati ndani ya Mahakama hususani unaohusiana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususani akili unde ili kushughulikia matatizo mbalimbali yaliyopo ndani ya Mahakama ambayo ni pamoja na mlundikano wa mashauri.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika kwa siku nne mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo ni pamoja na Majaji wanawake wanaongoza kuleta mabadiliko katika Mahakama za Kimataifa, Wanawake katika Uongozi-Mahali pa Kazi Usalama kwa Maafisa wa Mahakama, Ubaguzi na biashara haramu ya binadamu na nyingine.

Mada nyingine iliwasilishwa na Mhe. Edith Mwalukasa, Hakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo Tanzania mada hiyo ilijikita kuzungumzia ‘Athari za teknolojia katika masuala ya ukatili wa kijinsia.’ 

Aidha, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho, wanachama wa IAWJ walifanya uchaguzi na kumchagua Rais mpya wa Chama hicho ambaye ni Mhe. Maria Filomena D. Singh kutoka nchini Morocco.

Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili umeazimia kuwa, Mkutano ujao wa mwaka 2027 utafanyikia nchini Canada.

© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved

TAWJA YAWASILI CAPE TOWN KUSHIRIKI MKUTANO MKUU WA MAJAJI WANAWAKE DUNIANI

TAWJA YAWASILI CAPE TOWN KUSHIRIKI MKUTANO MKUU WA MAJAJI WANAWAKE DUNIANI

Jumla ya Majaji na Mahakimu Wanawake 43 ambao ni wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wamewasili katika Mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini leo tarehe 08 Aprili, 2025 kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani (IAWJ) unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 09 Aprili, 2025.
Akizungumza katika mahojiano maalum leo tarehe 08 Aprili, 2025 mjini humo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema kuwa, Mkutano huo unatarajiwa kuanza rasmi kesho tarehe 09 hadi 12 Aprili, 2025 na Mgeni Rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa.
“Mkutano huu ni wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Duniani, kwa ujumla unawakutanisha wanachama Majaji na Mahakimu wanawake duniani. Kwa upande wa Tanzania tutakaoshiriki katika Mkutano huo ni wanachama 43 idadi hii imejumuisha na wenzetu wa Zanzibar,” amesema Mhe. Sehel.
Kaulimbiu ya Mkutano huo inasema; ‘Wanawake na uongozi katika kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya dhidi ya wanawake.’
Mhe. Sehel amesema kuwa, mada mbalimbali zitawasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na Majaji wanawake wanaongoza na kuleta mabadiliko katika Mahakama za Kimataifa, Wanawake katika Uongozi-Mahali pa Kazi Usalama kwa Maafisa wa Mahakama, Ubaguzi na biashara haramu ya binadamu na nyingine.
Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano huo, mmoja wa washiriki watakaotoa mada ya ‘Athari za teknolojia katika masuala ya ukatili wa kijinsia’ ni Mhe. Edith Mwalukasa ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo.
Washiriki wa TAWJA wanaotarajia kuhudhuria mkutano huo ni baadhi ya wanachama ni kutoka kutoka Zanzibar, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Tabora na Mikoa mingine ya Tanzania Bara.

Mkutano wa aina hii huwakutanisha pamoja Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani kote na hufanyika kila baada ya miaka miwili na huwapa fursa Majaji hao kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki za wanawake, ukatili wa kijinsia, watoto na jamii kwa ujumla.

© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved