
MAKAO MAKUU YA TAWJA RASMI DODOMA
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema kuwa ofisi ya Makao Makuu ya chama hicho kwa sasa imehamia rasmi mkoani Dodoma.
Akiongoza kikao hivi karibuni cha wanachama wa TAWJA wa mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Mhe. Sehel alisema kuwa, hatua ya kuhamia Dodoma kutarahisisha mawasiliano, kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa urahisi lakini pia kukuza utendaji wa kisekta ndani ya mfumo wa haki nchini.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa neema yake ya kutufanya leo tumekutana hapa Dodoma na kuzungumza na wenzangu lakini pia nitumie fursa hii kuwajulisha kuwa kuanzia sasa ofisi ya TAWJA rasmi imehamia Dodoma na itakuwa katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama,” alisema Mhe. Sehel.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma ambaye pia ni Mlezi wa Chama hicho kwa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Juliana Masabo aliwapongeza wanachama wote na kuwakaribisha wanachama wengine katika Mkoa wa Dodoma na kuahidi kushirikiana nao kwa kila kitu.
Nao Wajumbe wa TAWJA Kanda ya Dodoma, walipongeza juhudi za viongozi wa chama hicho kwamba, hatua hiyo italeta fursa mpya katika kushirikiana, kuongeza ufanisi na maendeleo katika mfumo wa utoaji haki pamoja na shughuli nyingine za kijamii.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi kutoka Mahakama ya Rufani ambao ni Majaji wakiongozwa na Mwenyekiti wa TAWJA Taifa, Mhe. Barke Sehel, Mhe Patricia Fikirini, Mhe. Lucy Kairo, Mhe. Zainab Muruke, Mhe Leila Mgonya pamoja na viongozi wengine wanawake kutoka Mahakama.

TANZANIA WOMEN JUDGES ASSOCIATION.
Menu
© 2024 Tanzania Women Judges Association. All Rights Reserved